Lettera di Sant’ Ignazio di Antiochia ai Romani, in Swahili

Traduttore: Osuru, Marko Alisentus

Salamu

Ignasio (Ignatius), anayeitwa Theophorus, kwa Kanisa ambalo limepata huruma kupitia kwa Baba aliye na enzi kuu, na kwa mwanaye mpendwa, Yesu Kristu; Kanisa linalopendwa na kunuruhishwa kwa uwezo wake Mungu Baba, ambao umeumba vitu vyote kutokana na upendo wa Kristu Yesu, upendo ambao pia unapatikana kwa Warumi, Kanisa limstahiliyo Mungu, listahiliyo heshima, listahiliyo upendo mkuu, listahiliyo kusifiwa, listahiliyo kupata kila tamanio, listahiliyo kutakatifuzwa, na ambalo huishi daima katika upendo. Kanisa hilo limeitwa kutoka kwa Kristu na kwa Mungu Baba, ambalo pia nalisalimu kwa jina la Yesu Kristu, mwana wa pekee wa Mungu. Na kwa wale waliounganishwa pamoja kwa mwili na roho, na kwa amri zake Mungu, waliojazwa na neema ya Mungu na kusafishwa katika kila doa, yaani, dhambi, nawatakia baraka tele na upendo mkuu wa Bwana wetu Yesu Kristu.

Sura ya kwanza: Kama mfungwa natamani kukuona

Kwa njia ya sala kwa Mungu nimepata upendeleo wa kuuona uso wako uliotukuka, na kupewa zaidi ya kile nilichokiomba; kwa kuwa natumaini kama mfungwa katika Kristu Yesu kukusalimu, na kwamba kama kweli inastahili kulingana na mapenzi ya Mungu basi nifikiriwe kustahili kuendelea kuipata tunu hii hadi mwisho. Na kwa kuwa mwanzo tayari umeshapangiliwa na kufanywa vizuri, ninaweza kuendelea kupata neema ya Mungu ya kufikia matamanio na matumaini yangu bila ya kikwazo chochote hadi mwisho. Hakika naogopa upendo wako usije ukanifanyia na kuniachia majeraha, kwa sababu ni rahisi sana kwako kumaliza na kukamilisha kile ukipendacho; lakini ni vigumu kwangu kumfikia Mungu endapo utaniacha peke yangu.

Sura ya pili: Usiniokowe katika kifo shahidi (kifo dini)

Siyo matumaini yangu kutenda kwa kuwafurahisha watu, bali ni katika kumfurahisha na kumpendeza Mungu. Hivyo kwa kutokufanya jambo hilo wakati huu, hakika sitoweza kupata tena nafasi hii ya kumwona Mungu, na wala hata wewe mwenyewe hutoweza kuipata. Kama utabaki kuwa kimya, kamwe hutoweza kutunukiwa taji la heshima kwa kufanya kazi nzuri. Na endapo utakuwa kimya juu yangu, basi nitakuwa wa Mungu; lakini pia kama utaonyesha upendo wako kwa mwili wangu, pia bado nitapaswa kuendelea mbele na safari yangu. Omba, kisha usitafute kunifanyia msaada mkubwa juu yangu, bali uniombee niweze kutolewa sadaka kwa Mungu wakati meza (altare) yake ikiandaliwa; yaani, kuwekwa pamoja katika upendo, tukiimba nyimbo za sifa kwa Mungu Baba, kwa njia ya Yesu Kristu ya kuwa Mungu ameniokoa mimi Askofu wa Siria, nistahiliye kupelekwa mbali kutoka mashariki hadi magharibi. Hivyo basi, ni vema kutoka katika dunia hii kuelekea kwa Mungu ili niweze kufufuka upya katika Yeye (Mungu).

Sura ya tatu: Omba hasa ili niweze kufa shahidi

Hakika hujawahi kumchukiza mtu yeyote; umewafundisha wengine. Sasa napenda ya kuwa mambo hayo yote yaweze kuhakikiwa na kuonekana katika matendo yako, kwani ni kwa njia hiyo ya mafundisho na maelekezo yako kimatendo watu wengine watapata kujifunza pia. Hakika ni ombi litokalo ndani ya moyo wangu, ya kwamba nisiweze tu kuongea bali hilo liwe ni hitaji langu kufanya hivyo. Pia nisiitwe tu Mkristu bali Mkristu kweli. Na kama ni kweli ndivyo nilivyo, yaani, Mkristu kweli, basi niitwe hivyo na kisha kukombolewa kama mwaminifu pindi nitakapotoweka katika dunia hii. Hakuna kionekanacho chenye kuwa na umilele. Kwa sababu vitu vyote vionekanavyo kwa macho daima huwa ni vya kidunia, bali vile visivyoonekana huwa ni vya umilele, yaani huishi milele yote. Pia ukweli na uhalisia wa kuwa Bwana wetu Yesu Krstu yuko pamoja na Baba huonekana wazi kabisa katika utukufu wake. Na tukumbuke ya kuwa Ukristu siyo upole wala ukimya tu, bali ni ukuu katika kuyaishi yale yote tuliyofundishwa na kuachiwa na Bwana wetuYesu Kristu mwenyewe.

Sura ya nne: Niruhusu niwe chakula (mzoga) kwa mbwa mwitu wakali

Naandika kwa Makanisa ya kuwa kwa upendo na pasipokushurutishwa nitakufa kwa ajili ya Mungu. Niruhusu niwe chakula cha mbwa mwitu wakali, kwani kwa kufanya hivyo nitaweza kufika kwa Mungu. Mimi ni tunda la Mungu, hivyo basi, ni bora kwangu kutafunwa kwa meno ya hawa mbwa mwitu, ili niweze kuwa mkate ulio bora wa Kristu. Basi yafaa sana kwa hawa wanyama wakali kuwa kaburi langu, na bila kuacha hata sehemu moja ya mwili wangu ili nitakapolala usingizi wa milele, yaani kifo, nisiwe mzigo kwa mtu yeyote yule. Na kwa tendo hilo hakika nitakuwa mfuasi wa Kristu. Niombee kwa Kristu ili kwa kupitia njia hii niweze kuwa sadaka kwa Mungu. Sitowaamuru ninyi kama walivyokuwa Petro na Paulo; wao walikuwa Mitume, lakini mimi ni mshitakiwa; wao walikuwa huru, nami pia tena hadi sasa ni mfuasi wa Kristu. Lakini ninapoteseka hakika nitakuwa mtu huru wa Yesu Kristu, na nitafufuka pamoja naye. Na sasa kwa kuwa mimi ni mtumwa, najifunza kutokutamani na kutotaka mambo ya kidunia.

Sura ya tano: Natamani kufa

Kutoka Siria hadi Roma bado napambana na wanyama wakali, wa nchi kavu na wa majini, usiku na mchana, na kuzungukwa na kundi la vifaru kumi, yaani maaskari ambao japo hupata na kupokea faida kubwa huonekana kuwa wabaya. Lakini nafundishwa zaidi katika maumivu haya niyapatayo na kufanya zaidi kama mfuasi wa Kristu, japo bado sijathibitishwa kuwa hivyo. Naomba nifurahi kwa ajili ya hawa wanyama wakali walioandaliwa kwa ajili yangu; pia nasali ili waje kwangu na kuniraruwa haraka, na wala wasinifanye kama wengine ambao kwa uwoga hawakuweza kuwadhuru. Lakini pia kama hawatakuwa tayari kufanya hivyo basi nitawashurutisha. Mnisamehe katika hili kwani natambua wazi ni kitu gani kipo kwa faida yangu. Sasa naweza kuwa mfuasi wa Kristu. Basi na asiwepo mtu yeyote mwenye kinyongo ya kuwa mimi nitamwona Bwana wetu Yesu Kristu. Acha moto na msalaba, kundi la mbwa mwitu wakali, kuvunjika na kutengana kwa mifupa yangu, kukatwa na kutenganishwa kwa mwili wangu wote pamoja na mateso yote makali ya shetani yawe kwangu, ili tu niweze kufika kwa Yesu Kristu.

Sura ya sita: Kwa njia ya kifo nitapata uzima wa milele

Starehe zote za ulimwengu huu na ufalme wote wa duniani havitonifaidisha chochote. Ni bora kwangu mimi kufa kwa ajili ya Kristu kuliko kutawala katika pande zote za dunia. Basi yamstahili nini mwanadamu kama atapata kila kitu katika ulimwengu huu na kupoteza roho yake? Namtafuta Yeye yule (Kristu) aliyekufa kwa ajili yetu. Hakika hii ndiyo hazina niliyowekewa kwa ajili yangu. Naomba ndugu zangu msinizuie katika kuliishi hilo, na wala msinizuie katika hii hali ya kifo; na ninapotamani kuwa wa Mungu basi msinifanye kuwa wa ulimwengu huu. Mniruhusu kupata mwanga bora wa Kristu ili nitakapokuwa huko, yaani mbinguni, kweli niwe mwana wa Mungu. Mniruhusu niwe mfano bora wa mateso ya Kristu. Hivyo basi, kama kuna yeyote yule aliye naye (Kristu) ndani yake, basi na anifikirie kwa kile ninachokitamani, awe na huruma nami hasa akitambua ni kwa jinsi gani nateseka katika kumtafuta Kristu.

Sura ya saba: Sababu ya kutamani kufa

Ufahari wa ulimwengu huu waweza kunitenga mbali na kuharibu mahusiano yangu na Mungu. Hivyo basi na asiwepo mtu yeyote Roma kuja kunisaidia nisiweze kufa kwa ajili ya Kristu, bali mtu huyo na awe upande wangu, yaani awe upande wa Mungu. Pia si rahisi kuongea juu ya Yesu Kristu na kutoa maisha yetu kwake kama tutakuwa bado katika tamaa ya mambo ya kidunia. Kwa hiyo, tamaa na chuki visipate nafasi ndani mwako, wala hata mimi mwenyewe ninapokuwa pamoja nawe kukushawishi kunisikiliza, lakini zaidi ya yote yathamini mambo haya ninayokuandikieni sasa. Ijapokuwa mimi ni mzima na kuwaandikia, bado natamani kufa na hakika niko tayari kufanya hivyo. Upendo wangu umeshasulibiwa na hakuna tena ndani yangu msukumo unaohitaji kuongezwa, bali ndani yangu kuna maji yanayoishi na kuongea, maji yanayonena nami njoo kwa Baba. Sina hamu tena ya vyakula vya dunia hii wala hata starehe na fahari zote za duniani. Natamani mkate wa Mungu, mkate wa mbinguni, mkate wa uzima wa milele ambao ni mwili wa Yesu Kristu, mwana wa Mungu; pia natamani kinywaji cha Mungu, yaani damu ya Kristu ambayo ni upendo na uzima wa milele.

Sura ya nane: Uwe mwema kwangu

Sitegemei tena kuishi kulingana na matakwa ya watu, na hayo matamanio yangu yatakamilishwa na kuzaa matunda mema endapo utakubali na kuridhia kuwa mwema kwangu. Uwe tayari basi ili nawe pia matamanio ya hamu yako yaweze kukamilishwa. Kwa hivyo basi nakuomba walau unipongeze kwa hii barua fupi. Hakika Yesu Kristu atakufunulia mambo haya ninayokwambia ili tu uweze kutambua ya kuwa nasema ukweli. Kristu ni kinywa cha Mungu kisichosema uwongo, na ni kwa Yeye huyo Mungu ameweza kusema nasi. Niombee ili niweze kupata kile ninachokitamani, yaani kumwona Mungu. Sijawaandikieni kwa uwezo wangu, bali ni kwa uwezo na mapenzi ya Mungu. Na kama nitapata mateso basi ni kwa sababu ya matashi yenu mema, na endapo nitakataliwa basi mtakuwa mmenichukia mimi.

Sura ya tisa: Sali kwa ajili ya Kanisa la Siria

Katika sala zako na ukumbuke kuliombea Kanisa la Siria ambalo sasa Mungu ndiye mchungaji wake. Yesu Kristu mwenyewe ndiye atakaye lisimamia Kanisa hilo, na upendo wako pia kwa Kanisa hilo utalifanya kuwa imara. Mimi mwenyewe naona haibu kuhesabiwa kuwa miongoni mwao na hakika sistahili hata kuwa wa mwisho miongoni mwao. Mbali na hilo nimepata huruma ya Mungu. Roho yangu inawasalimu, na upendo wa Kanisa ambao umenipokea kwa jina la Yesu Kristu, na wala siyo kama mpitaji tu. Kwani hata yale Makanisa ambayo hayakuwa karibu au pamoja nami wamenitangulia wakipita mji hadi mji kuja kunilaki kwa furaha na shangwe tele.

Sura ya kumi: Hitimisho

Sasa nayaandika mambo haya kwenu kutoka Smyrna kwa Waefeso ambao kimsingi wanastahili kuwa na furaha kubwa. Pamoja nami wapo wengine wengi, Crocus ambaye pia ni mmoja wa wapendwa wangu. Na kwa wale wote walionitangulia kutoka Siria hadi Roma kwa ajili ya utukufu wa Mungu, naamini ya kuwa mliwaelewa vema walipowaambia juu ya ujio wangu. Kwa sababu wao ni wema kwa Mungu na kwenu pia; na kwa jinsi hiyo yawapasa kuwakumbuka kwa kila jambo. Nimeyandika mambo haya yote kwenu kabla ya siku ya tisa ya mwezi Septemba ( yaani siku ya ishirini na tatu ya mwezi Agosti). Nawaageni kwa upole na unyenyekevu wa Bwana wetu Yesu Kristu. Amina.